Exodus 18:13-27

Ushauri Wa Yethro

(Kumbukumbu 1:9-18)

13Siku iliyofuata, Mose akachukua nafasi yake kama hakimu wa watu, nao wakasimama kumzunguka kuanzia asubuhi hadi jioni. 14Baba mkwe wake alipoona yote Mose anayowafanyia watu, akasema, “Ni nini hiki unachowafanyia watu? Kwa nini wewe unakuwa mwamuzi wa watu hawa peke yako, wakati watu hawa wamesimama wakikuzunguka tangu asubuhi mpaka jioni?”

15 aMose akamjibu, “Kwa sababu watu wananijia kutaka mapenzi ya Mungu. 16 bKila wakiwa na shauri huletwa kwangu, nami huamua kati ya mtu na mwenzake na kuwajulisha juu ya amri na sheria za Mungu.”

17Baba mkwe wa Mose akamjibu, “Unachofanya sio kizuri. 18 cWewe pamoja na watu hawa wanaokujia mtajichosha bure. Kazi ni nzito sana kwako, huwezi kuibeba mwenyewe. 19 dSasa nisikilize mimi, nitakupa shauri, naye Mungu na awe pamoja nawe. Yapasa wewe uwe mwakilishi wa watu mbele za Mungu na ulete mashauri yao kwake. 20 eUwafundishe amri na sheria, tena uwaonyeshe namna ya kuishi na kazi zinazowapasa wao kufanya. 21 fLakini uchague watu wenye uwezo miongoni mwa watu wote, watu wanaomwogopa Mungu, watu waaminifu wanaochukia mali ya dhuluma, uwateuwe wawe maafisa juu ya maelfu, mamia, hamsini na makumi. 22 gWaweke wawe waamuzi wa watu kwa wakati wote, lakini waambie wakuletee kila shauri lililo gumu; yale yaliyo rahisi wayaamue wao wenyewe. Hii itafanya mzigo wako kuwa mwepesi, kwa sababu watashirikiana nawe. 23Kama ukifanya hivi, na ikiwa Mungu ameagiza hivyo, utaweza kushinda uchovu, nao watu hawa wote watarudi nyumbani wameridhika.”

Kuchaguliwa Kwa Waamuzi

24Mose akamsikiliza baba mkwe wake na kufanya kila kitu alichosema. 25 hMose akawachagua watu wenye uwezo kutoka Israeli yote, akawafanya kuwa viongozi wa watu, maafisa juu ya maelfu, mamia, hamsini na makumi. 26 iWakatumika kama waamuzi wa watu kwa wakati wote. Mashauri magumu wakayaleta kwa Mose, lakini yale yaliyo rahisi wakayaamua wenyewe.

27 jKisha Mose akaagana na Yethro baba mkwe wake, naye akarudi kwa nchi yake.

Copyright information for SwhNEN